Hapa Kazi Tu...JPM Aweka Rekodi ya Siku 25 bila Baraza la Mawaziri
Rais John Pombe Magufuli amekuwa wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini kutumia muda mrefu kutangaza Baraza la Mawazi kutok...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/12/hapa-kazi-tujpm-aweka-rekodi-ya-siku-25.html
Rais John Pombe Magufuli amekuwa wa kwanza tangu mfumo wa
vyama vingi kuanza nchini kutumia muda mrefu kutangaza Baraza la Mawazi
kutokana na kile wasomi, wachambuzi wa siasa kusema pengine anapata wakati
mgumu kupata mawaziri watakaoendana na kasi yake.
Katiba ya mwaka 1977 inamtaka Rais kumteua waziri mkuu
ndani ya siku 14 tangu alipoapishwa na kulipeleka jina lake bungeni, lakini
katiba hiyo ipo kimya kuhusu uteuzi wa mawaziri, hivyo Rais anaweza kutumia
muda wowote.
Wakati Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alipoingia madarakani
mwaka 1995 aliteua baraza la mawaziri Novemba 28, siku tano baada ya kuapishwa,
Jakaya Kikwete alitangaza Baraza la kwanza Siku 14 baada ya kuapishwa na Dk
Magufuli hadi sasa, siku 25 zimepita tangu aapishwe Novemba 5, mwaka huu
hajafanya hivyo.
Kazi ambazo Rais Magufuli ameanza kuzifanya bila mawaziri
ni kuzuia safari za nje, kuzuia sherehe za Uhuru na kuanza kupambana na
wabadhirifu wa fedha za umma.
Wasomi hao wakilinganisha alichokisema kwenye
hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge, walisema kuwa ana njozi za Tanzania aitakayo
huku akieleza wazi kuwa anatambua kuna mawaziri, wabunge wanakula rushwa na
akibainisha wazi hana imani kama waliomo ndani ya CCM wanakula pia.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Richard Mbunda, alisema kwenye mitandao ya kijamii kuna utani
unazunguka kuwa kwa kasi yake anaweza kufanya kazi hata bila kuwa na mawaziri.
“Ni utani, lakini ukiuchunguza mara mbili unaona kabisa
hata wananchi wameona anachokifanya na wanahitaji kukiona hicho kutoka kwenye
Baraza lake,” alisema. Alisema kasi yake na kubana matumizi alikoanza nako
anahitaji kuwa makini kwa sababu alitamka anataka kuwa na baraza dogo la
mawaziri.
Alifafanua kuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne mwaka
2005, mawaziri na naibu wao idadi yao ilikaribia 60, wakitumia mashangingi
yanayokula mafuta, posho, hivyo ili kudhibiti hilo atachukua muda pia, ikiwamo
kuvunja baadhi ya wizara kama ataona itafaa na kumsaidia anachotaka kukifanya.
