Biashara ya Dawa Maduka ya Muhimbili Yavurugwa
BIASHARA ya maduka ya dawa baridi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeingia shubiri, huku maduka mengine katika hospitali za Seri...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/biashara-ya-dawa-maduka-ya-muhimbili.html
BIASHARA ya maduka ya dawa
baridi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeingia shubiri, huku maduka
mengine katika hospitali za Serikali yakitakiwa kuwa tayari baada ya agizo la
Rais John Magufuli, kuanza kutekelezwa.
Dk Magufuli alipoingia madarakani tu,
moja ya maagizo yake alitaka Bohari ya Dawa (MSD) kufungua maduka ya dawa za
Serikali kwenye hospitali za rufaa na za kanda, ambapo kesho kutwa Jumatatu
duka hilo litaanza kufanya kazi Muhimbili na bei za dawa zitakuwa chini ya bei
ya soko.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laureane Bwanakunu, amesema kufunguliwa
kwa duka hilo kutaenda sambamba na kufunguliwa na duka lingine katika Hospitali
ya Kanda ya Mbeya na baadaye kwenye hospitali zingine za rufaa na kanda na
yatatoa huduma mpaka kwa wanaotumia utaratibu wa bima ya afya.
Kwa mujibu wa Bwanakunu, pia
MSD imeanza kuweka nembo ya Serikali kwenye vidonge na hadi sasa ina vidonge 45
ambavyo vimewekewa nembo ya GOT, ili kudhibiti wizi wa dawa za Serikali.
Bwanakunu amesema agizo la Rais la kuitaka MSD
kuanzisha maduka ya dawa karibu na hospitali hasa pale Muhimbili, limekuja
wakati muafaka. Alisema kwenye mpango mkakati wa miaka sita wa MSD, walikuwa na
malengo ya kufungua maduka hayo kwa ajili ya kusogeza huduma karibu kabisa na
wananchi.
“Agizo la Rais limetekelezwa
na duka la Muhimbili litafunguliwa Jumatatu, tunamalizia hatua zilizobaki na
mafundi wanafanya kazi usiku na mchana,” alisema na kuongeza kuwa duka hilo
ambalo litatumia mfumo wa risiti wa kielektroniki, tayari vibali vyake vyote
vimepatikana.
Bwanakunu alisema wamefanya
ziara ya kutembelea hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM) na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo,
Profesa Gesase Peter, ambaye aliahidi kuwapa eneo kubwa kwa ajili ya kuendeshea
duka hilo, litakalohudumia wateja wa Kanda ya Kati.
Mkurugenzi huyo alisisitiza
kuwa maduka ya MSD ambayo yatafunguliwa kwenye hospitali za rufaa na kanda,
yatafanya kazi saa 24 na kuuza dawa na vifaa tiba chini ya bei ya soko na
yatahudumia watu binafsi na wale waliopo kwenye taratibu za bima za afya.
Alisema maduka hayo
yataiongezea bohari wigo wa utendaji katika kutoa huduma kwa wananchi, tofauti
na sasa ambapo huduma ya dawa na vifaa tiba zinatolewa kupitia mali
zinazohifadhiwa katika bohari kupitia orodha ya taifa ya dawa na vifaa tiba
yenye aina ya dawa na vifaa tiba takribani 3,000 zinazoingizwa kwa mahitaji
maalumu.
Kuhusu udhibiti wa wizi wa
dawa, Mkurugenzi huyo alisema MSD inafanya kazi za uagizaji, uhifadhi na
usambazaji kwa kutumia mfumo wa mtandao wa E9.
“Lakini ili kudhibiti
upotevu wa dawa za Serikali tangu mwaka wa fedha uliopita tumeanza kuziwekea
alama ya GOT bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na vidonge, mkumbuke zamani ilikuwa
tunaweka kwenye vifungashio vya ndani na maboksi alama ya MSD,
lakini sasa hata kidonge
kina alama ya GOT, pale Dar es Salaam nina sampuli ya vidonge hivyo,” alisema.
Alisema vidonge ambavyo
tayari vimewekewa nembo ya GOT vipo 45 na wanaendelea kuwapa maelekezo
wazabuni, ili vyote viwekwe alama hizo. Akitaja aina za dawa zenye nembo ya
serikali, Mkurugenzi huyo alisema tayari dawa aina ya Diclofenac, Amoxillin,
Ciprofloxacin, Contrimoxale, paracetamol na magnesium.
Pia alisema sasa wataanzisha
huduma ya kutoa taarifa kwa njia ya simu ili wananchi watakapoona kuna wizi wa
dawa za Serikali, watoe taarifa na wananchi wataelimishwa kutoa taarifa pale
wanapoona dawa za serikali mitaani.
“Dawa nyingi zinaibwa kwenye
vituo ambavyo dawa zinapelekwa na sasa watatumia mfumo wa kompyuta kubaini wizi
wa dawa ambazo zimekuwa zikiibwa mkoa moja na kupelekwa mkoa mwingine.
“Rais Magufuli amesema
miongoni mwa vipaumbele vyake ni maji na dawa, MSD imejipanga kuokoa maisha ya
Watanzania,” alisema na kuongeza kuwa bajeti ya dawa ikiongezwa na kufikia Sh
bilioni 250 kila mtu atapata dawa.
Pamoja na jitihada hizo,
Bwanakunu alisema bado MSD inaidai Serikali fedha nyingi ambazo alisema tayari
wameanza kulipwa. “Tunaidai Serikali Sh bilioni 53 deni ambalo limehakikiwa na
majuzi tumelipwa Sh bilioni 14,” alisema.
chanzo:Habarileo
