Uchaguzi Zanzibar Wajadiliwa Bunge la Uingereza
Na Mwandishi Wetu HALI ya kisiasa na kufutwa kwa uchaguzi wa urais pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar hatimaye imetua...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/uchaguzi-zanzibarbar-wajadiliwa-bunge.html
Na Mwandishi Wetu
HALI ya kisiasa na kufutwa
kwa uchaguzi wa urais pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
hatimaye imetua na kujadiliwa katika Bunge la mabwanyenye la nchini Uingereza.
Uamuzi huo umekuja siku moja
baada ya wapinzani wawili wa kisiasa visiwani humo, Rais Dk. Ali Mohamed Shein
na Makamu wake wa Kwanza ambaye pia alikuwa mgombea wa urais kupitia CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad, kuendelea na vikao vya siri vinavyoshirikisha marais
wastaafu wa Zanzibar.
Sakata hilo liliibuka jana
nchini Uingereza katika kikao cha Bunge ambapo mbunge Lord Steel wa Aikwood
kutoka Chama cha Liberal Democrat, alitaka kujua tathmini ya Serikali ya
Uingereza kuhusu uchaguzi nchini Tanzania, hasa ule wa Zanzibar na
kilichoelezwa kwa Serikali ya Tanzania au Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola
kuhusu uchaguzi huo.
Kutokana na swali hilo,
Waziri wa Nchi, Baroness Anelay wa St. Johns, alisema kuwa pamoja na kuwapo
matatizo kadhaa, uchaguzi wa Tanzania ulifanyika kwa amani na uliendeshwa
vyema.
Alisema kutokana na hali
hiyo, Serikali ya Uingereza ilitoa pongezi kwa Rais Dk. John Magufuli kutokana
na ushindi wake alioupata katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
“Tulitoa pongezi zetu kwa
Rais Magufuli kufuatia ushindi wake. Hata hivyo, tulisikitishwa na uamuzi wa
kufuta uchaguzi wa urais na uwakilishi Zanzibar.
“Kwa nyakati tofauti
tulieleza masikitiko yetu kwa Serikali ya Tanzania kuhusu hilo, ikiwamo katika
ngazi za juu na hivi karibuni kabisa ilikuwa wiki iliyopita wakati wa mkutano
baina ya Balozi wa Tanzania mjini London na Waziri Mdogo wa Nchi kwa Masuala ya
Kigeni na Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Mbunge wa Rochford na Southend East,
James Duddridge,” alisema Anelay.
Pamoja na suala hilo la
kujadiliwa kwa uchaguzi wa Zanzibar nchini humo, lakini bado kumekuwa na
mazungumzo kadhaa ya kutafuta mwafaka wa suala hilo ambapo CUF kimekuwa
kikitaka matokeo yatangazwe na mshindi aapishwe, huku upande wa CCM, ukieleza
kuwa mazungumzo yanayoendelea hayazuii kufanyika kwa uchaguzi mwingine.
Mazungumzo hayo ya kutafuta
mwafaka wa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, yameendelea kufanyika
juzi Ikulu mjini Unguja.
Kikao hicho cha tatu
kilikuwa chini ya Dk. Shein, huku akimshirikisha Maalim Seif.
Taarifa kutoka Ikulu ya
Zanzibar zilieleza kwamba pamoja na kikao hicho kuwakutanisha mahasimu hao wa
kisiasa, pia kimehudhuriwa na wajumbe ambao ni marais wastaafu wa Zanzibar, Dk.
Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Matokeo ya mazungumzo hayo
yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi baada ya Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), kupitia Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, kutoa tamko la
kufutwa kwa uchaguzi huo, Oktoba 28, mwaka huu jambo ambalo liliibua mgogoro wa
kikatiba.
Novemba 9, mwaka huu,
mawaziri sita wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF walijiuzulu kutokana
na msuguano huo wa kisiasa visiwani humo.
Mgogoro wa kisiasa Zanzibar
umekuwa ukichukua sura tofauti, ambapo wiki iliyopita Wazanzibari wanaoishi
nchini Uingereza walifanya maandamano na kuitaka nchi hiyo iingilie kati na
kutoa shinikizo kwa Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha mshindi wa uchaguzi wa
rais wa Zanzibar anatangazwa na kuapishwa.
Wazanzibari hao walifikia
uamuzi huo kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, kutangaza kufuta
matokeo ya uchaguzi, huku akitoa sababu tisa ikiwamo uchaguzi huo kutokuwa huru
na haki.
Maandamano hayo yaliishia
katika Mtaa wa Downing zilipo ofisi za Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron
na kukabidhi barua yao.
Mbali na Uingereza,
Wazanzibari wanaoishi nchini Marekani nao pia waliandamana hadi Ikulu ya nchi
hiyo, ikiwa ni juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa ili kuupatia
suluhisho mzozo huo.
Akizungumza na waandishi wa
habari juzi mbele ya Ikulu hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari Waishio
Marekani (ZADIA) iliyoandaa maandamano hayo, Omar Haji Ali, alisema uamuzi wao
huo ni katika juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa katika kuukwamua
mgando wa kisiasa visiwani Zanzibar.
chanzo:mtanzania
