Maelfu Wauaga Mwili wa Mawazo Mwanza
Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Mh. Edward Lowassa akitoa h...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/maelfu-wauaga-mwili-wa-mawazo-mwanza.html
![]() |
Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Mh. Edward Lowassa
akitoa heshima zake kwa mwili wa Mawazo
|
MAELFU ya wananchi wa mkoa
wa Mwanza wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Taifa, Mhe. Freeman Mbowe wameuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti
wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo,
huku baadhi ya viongozi wa chama hicho,
wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu wakilitaka Jeshi la Polisi mkoani Geita
kuhakikisha watu waliohusika na mauaji ya kiongozi huyo wanakamatwa na
kufikishwa mahakamani mara moja.
Tukio la kuuaga mwili wa
marehemu Alphonce Mawazo katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza limetanguliwa
na ibada iliyoongozwa na Mchungaji Bernard Swai wa Kanisa la Winners.
Waziri Mkuu Mstaafu wa
serikali ya awamu ya tatu, Fredrick Sumaye pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa
Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), Mh. Edward Lowassa wakatoa angalizo kwa Jeshi la Polisi nchini
kuhakikisha linatenda haki katika kushughulikia kifo cha marehemu Alphonce
Mawazo.
Mtoto wa marehemu Alphonce
Mawazo, Precious Mawazo mwenye umri wa miaka tisa naye ametokea mbele ya
halaiki kuelezea majonzi ya kufiwa na baba yake mzazi.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa,
Freeman Mbowe naye akatoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Alphonce Mawazo,
aliyeuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana Novemba 14
mwaka huu katika Kijiji cha Katoro wilayani Geita.
Mwili wa marehemu Alphonce
Mawazo tayari umewasili mjini Geita ambako utalala usiku huu ili kutoa nafasi
kwa wananchi wa mkoa huo kutoa heshima zao za mwisho kesho Jumapili asubuhi ya
Novemba 29,
kabla ya kupelekwa nyumbani
kwao katika Kijiji cha Chikobe kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya
Jumatatu Novemba 30.

