CUF Yakanusha Kurudia Uchaguzi wa Zanzibar
KWA VYOMBO VYA HABARI Tumepokea taarifa kwamba Balozi Seif Ali Iddi amehojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International (...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/cuf-yakanusha-kurudia-uchaguzi-wa.html
KWA VYOMBO VYA HABARI
Tumepokea taarifa kwamba
Balozi Seif Ali Iddi amehojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France
International (RFI) na kusema kwamba eti viongozi wa CCM na CUF WAMEKUBALIANA
UCHAGUZI ZANZIBAR URUDIWE, na kinachojadiliwa hivi sasa ni NANI ASIMAMIE
UCHAGUZI WA MAREJEO kwa sababu ZEC ya JECHA INAONEKANA KUTOAMINIKA.
Tunapenda kuwawekea wazi
Wazanzibari wote kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote, ni za uzushi na
wazipuuze.
Msimamo wa CUF na Maalim
Seif Sharif Hamad uko pale pale kwamba HAKUNA KURUDIWA UCHAGUZI na kwamba
MSHINDI HALALI WA UCHAGUZI WA TAREHE 25 OKTOBA, 2015 ATANGAZWE NA KUAPISHWA.
Kauli za Balozi Seif Ali
Iddi ni za kutapatapa zianzolenga kuwatuliza wana-CCM ambao wanaonekana kukata
tamaa baada ya kushindwa vibaya na CUF kwenye uchaguzi mkuu wa Rais wa
Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Madiwani uliofanyika
tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kwenye uchaguzi mkuu wa
Urais wa Zanzibar, mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alimbwaga vibaya
mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa zaidi ya kura 25,000.
Balozi Seif Ali Iddi
mwenyewe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM anatuhumiwa na wana-CCM
kushindwa kazi na kukisababishia chama chao kushindwa vibaya kuliko wakati
wowote katika historia ya chaguzi za Zanzibar.
Lakini kama hilo halitoshi,
wana-CCM wanamtuhumu Balozi Seif na wajumbe wengine wa Kamati ya Kampeni
aliyokuwa akiiongoza kusimamia matumizi mabaya ya kiasi kikubwa cha fedha za
kampeni za Chama hicho ambazo sehemu kubwa walimdanganya mgombea wao, Dk. Ali
Mohamed Shein, kwamba zimetumika kuleta ushindi wa CCM kisiwani Pemba lakini
kumbe ziliishia katika mifuko ya watu binafsi.
Haistaajabishi kwamba sasa
Balozi Seif Ali Iddi ameamua kuja na njia ya kutoa taarifa za udanganyifu ili
kujinusuru na mzigo wa tuhuma za kushindwa kazi na kusimamia matumizi mabaya ya
fedha za kampeni kutoka kwa CCM wenzake.
CUF tunamtaka Balozi Seif
Ali Iddi awache kudanganya umma na badala yake awajibu CCM wenzake kwa nini
amekitia chama hicho aibu na fedheha kubwa ya kupata kipigo kibaya katika
uchaguzi kilichopelekea CCM kupoteza majimbo tisa (9) kisiwani Unguja na Dk.
Ali Mohamed Shein kushindwa uchaguzi wa Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura
25,000 huku wakidai kutumia mamilioni ya fedha ambazo hawana maelezo zimetumika
vipi.
CUF tunawataka Wazanzibari
kutobabaishwa na kauli za kushindwa kazi za Balozi Seif Ali Iddi na watulie
wakijua kuwa ufumbuzi wa haki wa uchaguzi mkuu utapatikana kwa kutangaza
matokeo ya kura kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye mshindi kutangazwa na
kuapishwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO –
CUF
26 NOVEMBA, 2015
