Zitto Aendelea Kuandamwa Zanzibar...Apewa Siku 14 Kuomba Radhi
Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amepewa siku 14 kufuta kauli yake na kuomba radhi kwa kumh...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/zitto-aendelea-kuandamwa-zanzibarapewa.html
Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amepewa siku 14 kufuta kauli yake na kuomba
radhi kwa kumhusisha rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na makosa ya
uhaini.
Msimamo huo ulitolewa na wagombea wawili wa nafasi ya
urais wa Zanzibar, Juma Ali Khatib (Tadea) na Soud Said Soud, walipokuwa
wakizungumzia kauli ya Zitto kudai haikuwa sahihi kwa Rais wa Zanzibar kubakia
madarakani wakati serikali yake imefikia ukomo wake Novemba 2, mwaka huu.
Soud alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Kifungu cha
28 (1)(a), Rais Shein ni Rais halali wa Zanzibar na atabakia madarakani
hadi atakapochaguliwa rais mpya kwenye uchaguzi wa marudio.
Alisema kuwa Dk. Shein alichaguliwa na wananchi wa
Zanzibar na haikuwa haki kwa Zitto kumhusisha na makosa ya uhaini kwa kuendelea
kubaki madarakani kwani yuko kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984. ‘Zitto Kabwe afute kauli yake na kuwaomba radhi wananchi wa Zanzibar
ndani ya siku 14 na asipofanya hivyo tutamfungulia mashitaka.’ alisema
Soud pia Mwenyekiti wa Chama cha AFP.
Katika sakata hilo, Juma Ali Khatib, alisema tayari
ameanza kutafuta namna ya kuwasiliana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ili kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya Zitto kwa kumhusisha na
makosa ya uhaini Rais wa Zanzibar.
Alisema iwapo Bunge litashindwa kumchukulia hatua za
kinidhamu Zitto, yeye atalazimika kufungua kesi kwa niaba ya wananchi wa
Zanzibar kupinga kauli ya Zitto.
Khatib alisema Zanzibar ni nchi na Rais wa Zanzibar
lazima apewe heshima yake kwa sababu kuendelea kuwepo kwake madarakani ni
matakwa ya Kikatiba.
‘Kumdhalilisha Rais wa nchi ni sawa na kutudhalilisha
wananchi wake, rais anashauriwa na vyombo vingi vya sheria hivyo hawezi kuvunja
Katiba,î’alisema Khatib
Viongozi hao si wa kwanza kujitokeza kumtetea Rais wa Zanzibar
kwani walitanguliwa na aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Rais ya Mabadiliko
ya Katiba, Simai Mohamed Said, tangu Zitto alipotoa kauli kuwa Zanzibar haina
rais na kuendelea kubakia madarakani Rais Shein ni sawa na kufanya uhalifu wa
uhaini.
Katika mkutano wake na wandishi wa habari hivi karibuni,
Zitto alisema kwa sasa Zanzibar haina serikali na mtu yoyote anayejiita rais wa
Zanzibar kikatiba amepindua nchi na katika hali ya kawaida anapaswa
kushitakiwa kwa uhaini.
chanzo:ippmedia
