Bunge Kuondoa Ajira za Kudumu Serikalini.....Kudumu Kwa Ajira Ya Mfanyakazi Kutategemea Juhudi Zake Kazini
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litafanyia mabadiliko makubwa sheria za utumishi wa umma kwa kuondoa ajira za kudumu serikalin...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/bunge-kuondoa-ajira-za-kudumu.html
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litafanyia mabadiliko
makubwa sheria za utumishi wa umma kwa kuondoa ajira za kudumu serikalini, ili
kuwezesha mabadiliko yaliyokusudiwa na Rais Dk. John Magufuli.
Katika mabadiliko hayo, mfumo sasa wa ajira za serikali kuwa za
kudumu utabadilishwa na badala yake, kudumu kwa ajira ya mfanyakazi kutategemea
juhudi na bidii yake kazini, ili kuondoa uzembe uliodumu miaka nenda miaka
rudi, katika sekta ya umma.
Akizungumza katika mahoajino binafsi na gazeti la Raia
Mwema, mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alisema baadhi ya sheria za kazi zinawafanya
baadhi ya watumishi wa umma kuwa wazembe.
“Kwa mfano katika serikali ya sasa mfanyakazi mzembe kabisa
kabisa hata waziri kumfukuza kazi hawezi. Hata Katibu Mkuu hawezi mpaka afuate
mlolongo mrefu na hatua nyingi sana, yaani kazi ni guarantee (uhakika) katika
nchi yetu ni permanent and pensionable (ya kudumu na ina pensheni). Sheria za
namna hiyo lazima ziondoke,” alisema Spika Ndugai .
“Katika nchi ambazo zinaendelea kwa haraka moja ya jambo ambalo
huna uhakika nalo ni ajira, ukifanya vizuri unayo ajira yako ukiboronga
unaondoka saa hiyo hiyo na wakati huo huo, sasa sheria za namna hiyo ni lazima
zibadilishwe ili watu wachape kazi. Wawe wakijua kabisa kwamba nipo kwa sababu
nachapa kazi akileta uzembe kazini kwaheri,”aliongeza.
Aliongeza kuwa mabadiliko mengine ambayo Rais Magufuli atayaleta
ni pamoja na ile sheria ya ununuzi na sheria nyingine ambazo ni za hovyo hovyo,
zinazoifanya serikali isifanye vizuri. Kwa mujibu wa Ndugai, Bunge
litahakikisha sheria hizo zibadilishwa haraka.
“Huo ndiyo ushirikiano wetu tutakaompa lakini pia tutachangia
vizuri katika mipango na bajeti zinazokuja tutazitengeneza vizuri zaidi kwa
kupunguza fedha zote za ulaji ulaji, hii ya kila mwaka mapazia, kuweka makochi,
kuweka makapeti na kompyuta kila mwaka na ofisi ni zile zile watu wale wale,
bajeti ilikuwa imejaa ununuzi wa magari vilainishi lazima tukate kote huko,” alisema.
Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Shirikisho la Vyama wa
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Gratian Mukoba, alisema hawezi kuunga mkono au
kukataa hoja hiyo mpaka atakapoona hoja yenyewe na maelezo yake.
“Kwa kawaida muswada wa sheria huanzia kwanza kwa wadau,
wakituletea tutaona, siyo kila kitu ni kibaya, sheria zinapotungwa zinakuwa na
sababu kwa nini zimetungwa. Unaweza ukawa na maelezo mazuri tukajadili
utekelezaji wake, tutaamua,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu mwenendo wa baadhi ya watumishi wa umma
kufanya kazi kwa mazoea na kama sheria hiyo inaweza kutibu tatizo hilo, alikiri
kuwepo kwa hali hiyo miongoni mwa watumishi wa umma lakini akatahadharisha
kwamba tiba yake siyo kuondoa ajira za kudumu.
“Ziko sababu nyingi zinazosababisha baadhi ya wafanyakazi kuwa
wazembe, siyo ajira ya kudumu peke yake. Kama kwenye nchi yenu mmeamua
kubaguana kwa malipo, mmoja analipwa mara 30 ya mwingine, huyo anayelipwa
kidogo hawezi kuwa na morali ya kazi, atanyong’onyea.
“Yule anayepata mara 30 ataathiriwa utendaji wake na hawa wenye
kidogo kwa sababu ni wengi, kwa sababu watajifanya (wanaolipwa kidogo) na
serikali itajifanya inalipa lakini kumbe kinacholipwa hakitoshelezi chochote,” alisema Mukoba.
Aliogeza kwamba miaka ya 1970 na 1980 watu walikuwa na uhakika
wa ajira za kudumu lakini walikuwa wanachapa kazi kwa bidii kwa kuwa kulikuwa
na uwiano wa haki kwenye malipo ya mishahara, tofauti na sasa, akishauri pia
suala la kushuka kwa morali ya kazi miongoni mwa watumishi wa umma lifanyiwe
utafiti makini na si kulikurupukia.
Chanzo: Raia Mwema
