Magogo Yenye Thamani ya Tsh milioni 300 Yakamatwa Dar
WIZARA ya Maliasili na Utalii imekamata makontena 31 ya magogo aina ya mitiki na misandali yenye thamani ya Sh milioni 300 yaliyokuwa y...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/magogo-yenye-thamani-ya-tsh-milioni-300.html
WIZARA ya Maliasili na Utalii
imekamata makontena 31 ya magogo aina ya mitiki na misandali yenye thamani ya
Sh milioni 300 yaliyokuwa yanasafirishwa kinyume cha sheria kwenda Mashariki ya
Mbali.
Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana katika eneo Nasaco yalikohifadhiwa makontena hayo,
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhelm Meru alisema watuhumiwa
walidai kuwa magogo hayo yalitoka Zambia na nyaraka husika zipo Tunduma.
"Tumebaini kuwa upo
mtandao wa kihalifu unaovuna rasilimali zetu za misitu kuandaa nyaraka bandia
za kusafirisha magogo nje ya nchi. Hata kama nyaraka hizo zingekuwepo ni batili
maana Tanzania hairuhusu uuzaji wa magogo nje ya nchi. Wahusika wote
watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria," alisema.
Aliongeza kuwa tayari ofisi
yake imeshawasiliana na TRA Tunduma kujiridhisha juu ya uhalali wa nyaraka hizo
(kama kweli zipo) ili kuufumua mtandao wote wa wizi na kufuatiwa na hatua zaidi
za kisheria.
Alisema uchunguzi wa awali
umebaini kuwa magogo yanavunwa kinyume cha sheria sehemu mbalimbali za nchi
kama Mbeya, Songea na kwingineko na wahusika kuandaa nyaraka za uongo kuonesha
kuwa magogo hayo yanatoka nje ya nchi.
"Leo hapa tunaye Balozi
Mdogo wa Zambia, Elizabeth Phiri ambaye amethibitisha pasi na shaka kuwa magogo
hayo hayajatoka nchini Zambia kama yeye mwenyewe alivyofafanua wakati wa
ukaguzi jijini Dar Salaam," alisema.
Balozi Phiri alisema Zambia
imepiga marufuku uuzaji wa magogo nje ya nchi hivyo nyaraka zinazodaiwa
kuonesha kuwa magogo hayo yanatoka Zambia hazitakuwa na uhalali wowote.
"Zambia hatuuzi magogo nje ya nchi bali tunauza mazao ya mbao. Tusubiri
tuone nyaraka zinazodaiwa kutoka Tunduma tuweze kupima ukweli wenyewe,"
Balozi Phiri alisema.
chanzo:Habarileo
