Maagizo ya Raisi Magufuli kuhusu Safari za Nje za Watendaji wa Serikali Yaanza Kutekelezwa
Kufuatia maagizo ya Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa hivi karibuni ya kusitisha safa...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/11/maagizo-ya-raisi-magufuli-kuhusu-safari.html
Kufuatia maagizo ya Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa hivi karibuni ya kusitisha safari za
nje kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa imeanza kutekeleza maagizo hayo kwa kutoa maelekezo
mahsusi kwa Balozi zake nje.
Wizara imezielekeza Balozi zote zilizopo maeneo mbalimbali
duniani kujipanga ili kushiriki kikamilifu katika kuiwakilisha Serikali kwenye
mikutano yote ya kimataifa na kikanda inayofanyika katika maeneo yao ya
uwakilishi. Tanzania inazo Balozi 35; Balozi Ndogo tatu; Vituo viwili vya
Biashara; na Konseli za Heshima 17 katika nchi mbalimbali. Hizi zote zitahusika
katika kuendeleza utekelezaji wa Diplomasia yetu ya Uchumi na uwakilishi wa
maslahi ya nchi yetu.
Aidha, hadi sasa Mikutano ambayo tayari imefanyika na Balozi
zetu kuwakilisha ni pamoja na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola
(CHOGM) unaoendelea nchini Malta na Mkutano wa Mawaziri wanaoshughulikia
masuala ya Habari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
unaofanyika nchini Lesotho.
Aidha, Wizara inatoa wito kwa Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali kuwasilisha mapema taarifa za mikutano inayohusu sekta zao ili kutoa
fursa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuzifanyia kazi
kwa wakati ili kuhakikisha ushiriki wa Tanzania unakuwa wenye tija kwa taifa.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaungana na
wadau wengine kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua za kuleta
ufanisi mkubwa wa kazi na kubana matumizi ili kuiwezesha Serikali kuwahudumia
wananchi kikamilifu.
Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
27 Novemba, 2015
