Viongozi Wakuu wa NCCR - Mageuzi Waikosoa UKAWA
UTANGULIZI Sisi viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu tukiwa na Wajumbe wa Halmashauri K...
http://taarifayahabari360.blogspot.com/2015/09/viongozi-wakuu-wa-nccr-mageuzi-waikosoa.html
UTANGULIZI
Sisi viongozi wa ngazi
ya juu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu tukiwa na
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa na viongozi wengine, tumekuja mbele yenu
mtusaidie kufikisha ujumbe maalum kwa wanachama wetu na Watanzania wote wanaokiamini
chama chetu,.
Tumefika kuelezea kutoridhishwa na mwenendo wa ushirikiano wa
vyama vinavyounda UKAWA. Tumekuja pia kuwaelezea ni hatua gani tulizoamua
kuchukua kukabiliana na changamoto hii.
Wengi wenu mnafahamu kuwa UKAWA ni Umoja wa Katiba ya Wananchi
ulionzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba kutetea Rasimu ya Katiba
iliyotokana na maoni ya wananchi dhidi ya uchakachuaji uliokuwa unafanywa na
CCM.
UKAWA siyo chama cha siasa bali umoja. NCCR-Mageuzi iliamua
kujiunga na harakati hizi kwa nia njema ya kutetea maslahi ya taifa letu.
Zaidi ya mwaka sasa tangu tujiunge na umoja huu, matokeo yake yamekuwa ni mabaya kwa uhai na ustawi wa chama chetu. Wakati vyama vingine vimezidi kuimarika ndani ya UKAWA, NCCR-Mageuzi imedhoofika. Hali hii haikubaliki.
Zaidi ya mwaka sasa tangu tujiunge na umoja huu, matokeo yake yamekuwa ni mabaya kwa uhai na ustawi wa chama chetu. Wakati vyama vingine vimezidi kuimarika ndani ya UKAWA, NCCR-Mageuzi imedhoofika. Hali hii haikubaliki.
MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO BAINA YA VYAMA VYA UKAWA
Vyama vinavyounda UKAWA, vilisaini Makubaliano ya Ushirikiano
katika Mkutano wa Hadhara kwenye viwanja vya Jangwani. Kitendo hicho
kiliwavutia na kuwapa matumaini wananchi na wao wakazidi kutuunga mkono.
Iliamuliwa kwamba tusiuwe vyama vyetu bali tuunganishe nguvu za vyama vyetu
kama namna ya kujiimarisha kwa pamoja.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA DISEMBA 2014.
Kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, vyama
vinavyounda UKAWA vilitiliana saini ya Mwongozo wa Ushirikiano katika Uchaguzi
huo.
Licha ya kutiliana saini Makubaliano hayo, bado kulikuwa na
ukiukwaji mkubwa na wa makusudi wa Mwongozo huo.
Licha ya kuzijadili changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi
huo, lakini hazikupatiwa ufumbuzi wowote.
Sisi tuliopo hapa tulionya mapema kuhusu mwenendo huu wa kuvunja
makubaliano na tukaomba taratibu tulizokubaliana zitumike ili kurudi kwenye
misingi ya UKAWA lakini hatukusikilizwa.
USHIRIKIANO KATIKA UCHAGUZI MKUU, OKTOBA 2015.
Licha ya changamoto zilizokuwepo, tuliamua kwa pamoja kwamba
vyama vya UKAWA tuingie katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na makubaliano ya
ushirikiano, ikiwemo kuwa na mgombea mmoja wa Urais na kuachiana majimbo ya
uchaguzi.
Pia, katika kuendesha umoja huu, tuliunda vyombo vya kutusaidia
ambavyo ni:-
1.
Kamati ya Wenyeviti.
2.
Kamati ya Makatibu Wakuu.
3.
Kamati ya Ufundi.
4.
Kamati ya Wataalam.
Pamoja na kuunda vyombo vya kuendesha UKAWA, tangu Januari 2015,
bado tumeshindwa kujenga UKAWA imara na tuliyotarajia kwa manufaa ya wanaukawa
na wananchi kwa ujumla.
Yafuatayo yamethibitisha hili jambo:
1.
Tumeshindwa kuweka
Kanuni za uendeshaji wa UKAWA kama tulivyokubaliana. Kwa maana hiyo, tunafanya
mambo kiholela
2.
Tumeshindwa kuunda
Kamati zitakazoshughulikia migogoro baina ya vyama.
3.
Tumeshindwa kuunda na
kuzisimamia Kamati za Majimbo
4.
Tumeshindwa kupata
muafaka wa kuachiana majimbo.
Mfano, NCCR – Mageuzi tuliachiwa majimbo 12 ya Kasulu Vijijini,
Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini, Manyovu,
Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe mjini. Ikumbukwe kwamba, mwaka 2010,
NCCR-Mageuzi ilisimamisha wagombea katika majimbo 67.
Kwa maana hiyo, UKAWA umeturidisha nyuma katika kupata wabunge
na kuimarisha chama zaidi ya miaka 20 baada ya kuundwa kwake.
Licha ya kukubaliana kwamba NCCR-Mageuzi iachiwe majimbo 12,
wenzetu wa vyama vingine katika UKAWA wamesimamisha wagombea katika majimbo 6
kati ya hayo. Wametuvunja moyo na kutuonyesha kwamba hawatujali. Na hata kule
ambapo katika majimbo sita ambapo wametuachia bado wenzetu wanatufanyia fujo
kuliko hata wanazotufanyia wanachama wa CCM. Tunamifano mingi ya kuonyesha ni
jinsi gani wagombea wetu wanavyofanyiwa vurugu.
1. Tumeshindwa kupata
muafaka wa namna ya kuachiana wagombea udiwani katika kata nyingi.
2.
Tumeshindwa kuonesha
na kukubaliana kila chama kitapata nafasi gani na ngapi katika Serikali ya
UKAWA.
3. Tumeshindwa kufuata
utaratibu wa kumpata mgombea Urais wa UKAWA
4. Tumeshuhudia vurugu
kubwa iliyoletwa ndani ya UKAWA na wanachama waliotoka CCM na wao kupewa
umuhimu kuliko viongozi wa UKAWA. Zaidi ya Mbatia hakuna kiongozi wa
NCCR-Mageuzi anayeshirikishwa, anayezungumza au aliyepo kwenye kampeni za
mgombea Urais wa UKAWA.
5. Tumeshindwa kuwa na
timu ya kampeni timu ya UKAWA, ambayo inagharamiwa na UKAWA na inatafuta fedha
pamoja, kama ilivyokubaliwa.
6. Tunashuhudia UKAWA
ambayo Chadema ndiyo UKAWA-Bara na CUF ndio UKAWA-Zanzibar. Chadema haijali
Zanzibar na CUF haijali Bara. Na NCCR-Mageuzi haipo huku wala kule ikiendelea
kudhoofika siku hadi siku.
7. Tumeshindwa
kuona uwazi katika matumizi ya fedha na maamuzi muhimu ya uendeshaji wa UKAWA.
8. Tumefadhaishwa
na kuvunjwa kwa misingi ya kuanzisha kwa UKAWA.
9. Wakati NCCR imetii
mgawanyo wa majimbo kwa vyama vinavyounda UKAWA, vyama vingine na hasa CHADEMA
vimesimamisha wagombea kinyume cha makubaliano.
NINI KIFANYIKE NA UKAWA
Hatukuwaita hapa kuwaambia kwamba tunajiuzulu siasa kutokana na
changamoto hizi. Tumeamua kupambana na kurudisha hadhi na heshima ya Chama
chetu. Hatuwezi kubwaga manyanga.
Tunataka kuitoa CCM madarakani kutokana na ulaghai na ujanja-ujanja wa miaka 50. Lakini hatuwezi kuitoa CCM kwa mbinu za ulaghai na ujanja-ujanja. Tunakwenda kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na Watanzania. Tunao wajibu wa kujiongoza vizuri ili tuwaonyeshe Watanzania kwamba tuna uwezo wa kuwaongoza vizuri.
Tunataka kuitoa CCM madarakani kutokana na ulaghai na ujanja-ujanja wa miaka 50. Lakini hatuwezi kuitoa CCM kwa mbinu za ulaghai na ujanja-ujanja. Tunakwenda kukabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi na Watanzania. Tunao wajibu wa kujiongoza vizuri ili tuwaonyeshe Watanzania kwamba tuna uwezo wa kuwaongoza vizuri.
WITO WETU
1. Tunamshauri Mwenyekiti
wetu, ndg. James Mbatia, aitishe vikao vya kikatiba ili tuweze kujadiliana
kuhusu hatima ya chama chetu.
2. Tunashauri ndg. Mbatia
asiwemsemaji wa CHADEMA wakati anakiacha chama chake (NCCR-Mageuzi)
kinadhoofika. Kwa mfano, Dr. Slaa alipoishambulia Chadema hakuna kiongozi wa
Chadema aliyemjibu isipokuwa Mbatia ndiye aliyeamua kujiingiza kwenye ugomvi
ndani ya Chadema.
3. Tutachangishana ili
tusafiri kwenye majimbo na kata za wagombea wetu na kuwasaidia kwenye kampeni
ili wasibaki wapweke kama yatima.
Tunasisitiza kwamba upinzani wa kweli nchini hauwezi kujengwa
kwa njia za hila, kwa kukiuka taratibu za kidemokrasia tulizojiwekea wenyewe,
kwa kukiuka misingi muhimu kama uadilifu, kwa kuweka mbele tamaa na maslahi
binafsi kuliko taifa, kwa kutegemea propaganda. Tukifanya hivi, wananchi
watashindwa kututoufautisha na CCM na wataamua kuchagua zimwi walijualo. Hatari
hii tunaiona wazi kabisa.
……………………………
Leticia Ghati Mossore
Makamu Mwenyekiti (Bara)
NCCR-Mageuzi
17.09.2015
Mosena Nyambabe
Katibu Mkuu, NCCR Mageuzi
