Chadema Waigaragaza Polisi Mazishi ya Mawazo

Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imemaliza utata kuhusu kuagwa ama kutoagwa jijini Mwanza kwa mwili wa marehemu Alphonce Mawazo, aliyekuwa ...


Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imemaliza utata kuhusu kuagwa ama kutoagwa jijini Mwanza kwa mwili wa marehemu Alphonce Mawazo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Geita.

 Jaji Lameck Mlacha, alitoa uamuzi juu ya shauri hilo mahakamani hapo jana, akisema marehemu Mawazo ana haki ya kikatiba kuagwa na kufanyiwa ibada Mwanza, ambako baba yake mdogo anaishi.

Uamuzi huo ulitolewa kutokana na ombi la muombaji ambaye ni baba mdogo wa marehemu, Charles Lugiko dhidi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatia zuio la mwili huo kuugwa jijini Mwanza.
Hukumu hiyo iliyoanza kusomwa saa 7:30 mchana na kuhitimishwa saa 8:22 mchana. 

Jaji Mlacha alisema baada ya kupitia maombi ya mapitio ya muombaji (Lugiko) dhidi ya kamanda wa polisi kwa ajili ya hati ya dharula, ameona kuna kasoro katika zuio hilo.Alisema kifungu 30 (3) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

kinachozungumzia haki ya msingi ya raia, kinasema mtu yeyote anayeona haki yake imeingiliwa au kuvunjwa, anaweza kwenda Mahakama Kuu ili kuweka zuio.
Jaji Mlacha alisema kwa mujibu wa kifungu cha 19, marehemu ana haki ya kuagwa na ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa chama chake na pia kufanyiwa ibada kutokana na imani yao.

Alisema alichofanya kamanda wa polisi hata wanasheria wa serikali waliomwakilisha walikubaliana mwili huo kuagwa Mwanza, lakini walichopinga ni namna ya uagaji wake ulivyopangwa. “Mtu asiangaliwe kwa historia yake ya nyuma, bali kinachotakiwa aangaliwe kwa muda uliopo sasa…

Mawazo anaangaliwa zaidi kisiasa kwa ngazi ya kitaifa, pia mlezi wake anaishi Mwanza,” alisema Jaji Mlacha.

Jaji Mlacha alisema si jambo geni kwa mtu kufariki sehemu nyingine, kuagwa sehemu nyingine na kuzikwa sehemu nyingine, hivyo marehemu Mawazo ana haki ya kikatiba kuagwa na kufanyiwa ibada Mwanza ambako baba yake mdogo anaishi.

Jaji huyo alisema, iwapo polisi waligundua kutakuwa na vurugu wakati wa uagaji wa mwili huo jijini Mwanza, wasingetoa amri ya zuio kwani walifanya hivyo wakijua wanaondoa haki kikatiba. “Kamanda wa polisi ana haki ya kuwaita ndugu na viongozi wa Chadema na kuzungumza nao na wala si kuwanyima haki yao kikatiba…haki ya kisheria ilikuwa ni kuwaita wote na kukubaliana,” alisema.

Aidha, Jaji Mlacha alisema kifungu cha 5 (1) kilichotumiwa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu, Seth Mkemwa, kuwa kamanda wa polisi ana haki hiyo, si kweli kwani kifungu hicho hakimpi mamlaka polisi kufanya hivyo zaidi ya kulinda amani.

“Hivyo, amri iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza si sahihi na Mahakama Kuu inafutilia mbali mamlaka hiyo ya kamanda,” alisema. Baada ya kutoa hukumu hiyo, Jaji Mlacha alitoa maelekezo kwa muombaji na viongozi wa Chadema kukutana na kamanda wa polisi mkoa haraka ili wapange jinsi ya kufanya ibada na kisha kuaga mwili wa marehemu.

Pia alimtaka kamanda wa polisi azingatie hukumu hiyo iliyotolewa pamoja na kutakiwa kuweka ulinzi ili watu waweze kufanya ibada na kuaga pasipokuwapo na silaha nzito.

JAJI AWAONYA CHADEMA
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa Chadema wakati wa shughuli hiyo kujiepusha na kauli zinazoweza kuchochea hasira za wafuasi wa chama hicho kwani marehemu ameuawa na watu wasiojulikana.

“Nawaomba viongozi wa Chadema wajizuie kutoa kauli za kuleta mihemko kwa wafuasi wa chama chao kutokana na marehemu kuuawa na watu wasiojulikana,” alisema. 


chanzo:ippmedia

Related

Kitaifa 5740615695451352441

Post a Comment

emo-but-icon

Hot in week

Recent

Comments

Side Ads

Text Widget

Connect Us

item